Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi Kamishna Msaidizi wa Polisi ACP Elisante Mmari amewataka wananchi kutojichukulia sheria mikononi pindi wanapombaini au kumkamata mtuhumiwa kwani kufanya hivyo ni kosa kisheria.
Kamanda Mmari ametoa kauli hiyo tarehe 27 Septemba 2024 wakati akizungumza na wanamichezo na wananchi walioshiriki katika fainali za mpira wa miguu za Polisi Jamii Cup Wilaya ya Mjini.
Amesema wananchi wamepewa mamlaka kisheria kukamata wanapoona mtu anafanya kosa la jinai mbele yao, hivyo amewasisitiza kutotumia takwa hilo kinyume na sheria.
“Pamoja na takwa la kisheria kuwatambua wananchi kufanya ukamataji, ni jukumu lenu kuwafikisha watuhumiwa hao mbele ya Jeshi la Polisi ili hatua nyingine za kisheria zichukue mkondo wake” alisema Mmari.
Pia amewataka kutumia dhana ya Polisi Jamii kama sehemu ya kukomesha vitendo vya kihalifu katika jamii kwa kushirikiana na Polisi Shehia waliopo kwenye maeneo yao ambao wanawajibika kuzuia vitendo vya aina yoyote vinavyoenda kinyume na sheria.
Nae Mkuu wa Polisi Wilaya ya Mjini Mrakibu Mwandamizi wa Polisi SP Bakar amepongeza ushirikiano wa wananchi kwa Jeshi la Polisi katika kipindi chote cha mashindano hayo ambayo yalishirikisha timu 16 za mpira wa miguu.
Mchezo huo wa fainali umechezwa majira saa 10:30 alasiri katika Uwanja wa Mao Zedong Zanzibar ambapo fainali hiyo ilichezwa kati ya Mwembe Makumbi City dhidi ya Ziwatuwe City ambapo katika mchezo huo timu ya Ziwatuwe iliibuka kidedea baada ya kuitandika goli 1 – 0, goli ambalo lilidumu kwa dakika 90 hadi kumalizika kwa mchezo huo.
Mshindi wa kwanza wa fainali hizo Ziwatuwe City alikabidhiwa zawadi ya fedha Shilingi 1,000,000 mipira miwili pamoja na jezi seti moja. Mshindi wa pili alikabidhiwa fedha shilingi 500,000 jezi seti moja na mipira miwili.
Mapema mchezo wa mshindi wa tatu ulichezwa kati ya Town Boys Fc dhidi ya FFU Mjini ambapo timu ya Town Boys iliibuka na ushindi wa mikwaju ya penati 3 – 2.
Mshindi wa tatu alikabidhiwa zawadi ya fedha shilingi 300,000 seti ya jezi pamoja na mipira miwili.
This post was created with our nice and easy submission form. Create your post!
GIPHY App Key not set. Please check settings